Leviticus 10

Kifo Cha Nadabu Na Abihu

1 aNadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea Bwana moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu. 2 bHivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Bwana na kuwaramba, nao wakafa mbele za Bwana. 3 cKisha Musa akamwambia Haruni, “Hili ndilo alilonena Bwana wakati aliposema: “ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia
nitajionyesha kuwa mtakatifu;
machoni pa watu wote
nitaheshimiwa.’ ”

Haruni akanyamaza.

4 dMusa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Haruni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya binamu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.” 5 eHivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Musa alivyoamuru.

6Ndipo Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na Bwana ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao Bwana amewaangamiza kwa moto. 7 fMsitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya Bwana ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Musa alivyosema.

8Kisha Bwana akamwambia Haruni, 9 g“Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa Agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 10 hNi lazima mtenganishe kilicho kitakatifu na kile kilicho cha kawaida, kati ya yaliyo najisi na yaliyo safi, 11na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo Bwana aliwapa kupitia Musa.”

12 iMusa akamwambia Haruni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana. 13Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa. 14 jLakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila mahali safi pa kawaida ya ibada; mmepewa wewe na watoto wako kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli. 15 kPaja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za Bwana kama sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako la kawaida na wanao, kama Bwana alivyoagiza.”

16 lMusa alipouliza kuhusu mbuzi atolewaye kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kukuta kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni waliobaki, akawauliza, 17 m“Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za Bwana. 18 nKwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.”

19 oHaruni akamjibu Musa, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za Bwana, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, Bwana angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?” 20Musa aliposikia haya, akaridhika.
Copyright information for SwhKC